Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wananchi wa Wilaya ya Misungwi hususan vijana wa maeneo ya karibu na mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo –Busisi kuchangamkia fursa za ajira ili kuongeza kipato na hatimaye kupata maendeleo.
Rais Magufuli amesema hayo leo wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi ambalo litakuwa na urefu wa kilomita 3.2 kwenye Ziwa Victoria, linalounganisha Wilaya ya Sengerema na Misungwi, Mkoani Mwanza.
“Natoa wito kwa Wananchi wa karibu wapewe kipaumbele ili watumie fursa hii kupata ajira, wakiwemo vijana na mama lishe ili waweze kuongeza kipato na kujiletea maendeleo yao binafsi na familia zao,”alisema Rais Magufuli, pia amemtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati hivyo wafanye kazi usiku na mchana,
Rais Dkt, John Pombe Magufuli akikata utepe katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi Wilayni Misungwi.(wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Kamanda,Simon Sirro, na wa pili kushoto ni Mkuu wa Majeshi ya ulinzi nchini Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo pamoja na Mama Janety Magufuli Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (kulia)
Baadhi ya Wananchi wakiwemo Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi waliofurika kwa ajili ya kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Kigongo - Busisi (wa kwanza kulia ni Mwamba Makune Diwani wa Kata ya Misungwi)
Rais Magufuli amesema mradi huu unatekelezwa kwa fedha za ndani ya nchi na kubainisha baadhi ya manufaa ya mradi ni pamoja na kujenga uchumi na kukuza biashara za nchi mbalimbali za Rwanda, Burundi na Congo, kuondoa kero ya usafiri kwa kutumia masaa zaidi ya mawili na nusu kwa Kivuko kwa sasa, ambapo kwa kutumia Daraja itakuwa unatumia dakika 4 tu, na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa haraka.
Rais Dkt, John Pombe Magufuli amesema Serikali imetenga fedha shilingi Bilioni 3.45 kwa ajili kulipa fidia kwa Wananchi wote waliopitiwa kwenye maeneo ya mradi huu kwa mujibu wa sheria za Ardhi na fedha hizo zitatolewa mapema, pia amewaonya Wananchi watakaojitokeza kudai madai ya udanganyifu yasiyokuwa halali kwani malipo ya fidia yanahusu yule aliyekutwa na barabara na siyo aliyefuata barabara.
Awali, akiwasilisha taarifa ya mradi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi , Mhandisi Issack Kamwelwe amesema kwamba ujenzi wa mradi wa Daraja la Kigongo – Busisi utahusisha pia barabara unganishi ya lami yenye urefu wa kilomita 1.66 ambapo gharama ya ujenzi wa mradi wote utakuwa ni shilingi Bilioni 699. 2 fedha za kitanzania.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa barabara TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale amesema kwamba tayari Mkandarasi toka nchini China ameshaanza kazi ya ujenzi wa daraja hili ambalo litakuwa la njia nne (4) na litajengwa kwa ubora zaidi na matarajio ya kudumu kwa zaidi miaka 100, ambapo daraja hili lina urefu wa kilomita 3.2 ambalo litakuwa daraja la kwanza kwa ukubwa kwa nchi za Afrika Mashariki na hivyo kuwa daraja la sita kwa Afrika nzima.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.