Naibu Waziri wa TAMISEMI, Josephat Kandege aipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kutoa Mikopo ya shilingi 298,117, 000 /= toka Mapato ya ndani kwa vikundi mbalimbali vya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu kuanzia mwaka Julai 2018 hadi machi mwaka huu. .
Akizungumza na Viongozi wa ngazi ya Wilaya wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani Misungwi, Mhe, Josephat Kandege amewapongeza Viongozi na Watendaji wote kwa juhudi na mipango thabiti katika kusimamia miradi ya Vikundi vya Vijana, Walaemavu na Wanawake inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
“ katika mambo ambayo nina kila sababu na nazidi kuupongeza Uongozi wa Wilaya na Halmashauri hii, ni namna ambavyo wameweza kusimamia vizuri zoezi la utoaji wa Mikopo ya asilimia 10 ya fedha zitokanazo na mapato ya ndani, kimsingi nimesikia katika Halmashauri za Mkoa wa Mwanza, hawa ndo wamekuwa wanatoa zaidi ya shilingi milioni 45 katika vikundi viwili, hatuwezi kuendelea kutoa shilingi milioni moja moja ambazo haziwezi kutufikisha mbali,” alieleza kwa msisitizo Naibu Waziri Kandege.
Ametoa wito na kuwahimiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri zingine nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Misungwi katika suala la utoaji wa mikopo hii, tunatarajia mikopo hii itatoa fursa za ajira kwa vijana wengi na kuweza kuwasaidia mamilioni ya Watanzania na kuachana na habari na utaratibu wa kutoa mikopo ya milioni moja moja ambayo haiwezi kuwasaidia Wananchi kuinua uchumi na kujikwamua na umasikini.
Mhe, Kandege amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha mikopo ya vikundi inarejeshwa kwa wakati ili ziweze kukopeshwa kwa wengine na kuwaomba kukopesha mikopo hiyo kwa vikundi ambavyo vinaweza kufanya miradi mikubwa kama Kikundi cha Usagara Gypsum Group ambacho kinatengeneza Mikanda ya Gypsum pamoja na Chalk Wilayani Misungwi na kuwasimamia kuwawezesha vizuri ili waweze kurejesha mikopo vizuri.
Akitoa taarifa ya Wilaya ya maendeleo ya utoaji wa Mikopo kwa vikundi Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya, Willehimina Nkunga amesema kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, kwa kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Machi 2020 imefanikiwa kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali 45 vya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu wenye shilingi milioni 298,117,000/= kwa ajili ya kuanzisha miradi ya maendeleo.
Bi, Nkunga amesema kuwa Halmashauri imetoa mikopo katika Vikundi 45 ambavyo ni vikundi vya Wanawake 24, Vikundi vya Vijana 15, na Vikundi vya watu wenye Ulemavu 6 na kueleza kwamba wameviwezesha mikopo wa shilingi milioni 45,000,000/= vikundi viwili vya Vijana ambavyo ni Kikundi cha Usagara Gypsum Group shilingi milioni 11,000,000/= za mradi wa Kiwanda kidogo cha kutengeneza Mikanda ya Gypsum pamoja na mkopo wa kununua mashine ya kutengeneza Chalk shilingi milioni 13,500,000/=, pia Kikundi cha Mabuki Vijana Maendeleo walipewa mkopo wa shilingi milioni 22,600,000/= kwa ajili ya mradi wa Kiwanda kidogo cha kusindika maziwa, ambapo uzalishaji umeshaanza tayri.
Ameongeza kuhusu marejesho ya mikopo hiyo kwa walemavu , Wanawake na Vijana wameshaanza marejesho na kwamba kwa vikundi vya Vijana yanaendelea vizuri na Idara ya maendeleo ya jamii inaendelea kuratibu na kufuatilia marejesho hayo na kuhakikisha yanafanyika kwa wakati.
Katika ziara ya Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe, Josephat Kandege Wilayani Misungwi, ameweza kukagua na kuona shughuli za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo na Ukarabati wa Jengo kwa ajili ya Soko la Madini, mradi wa Ufyatuaji wa matofali wa Halmashauri, mradi wa Kiwanda cha kutengeneza mikanda ya Gypsum na Chalk Usagara, mradi wa barabara ya Nyashishi – Fella ambapo ameridhishwa na kazi zinazoendelea.
Mmoja wa Wanakikundi wa Kikundi cha Usagara Gypsum Group kinachotengeneza Mikanda ya Gypsum akiandaa Nyuzi kwa ajili ya kutengeneza mkanda wa Gypsum wakati Mhe, Naibu Wazuri wa TAMISEMI alipotembelea kuona shughuli za kikundi hicho eneo la Usagara Wilayani Misungwi.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.