MKUU WA WILAYA AAGIZA WATENDAJI WA HALMASHAURI KUKUSANYA MAPATO YA USHURU WA MADINI YA DHAHABU NA ALMASI
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe,Juma Sweda amewataka Watendaji wa Halmashauri kufuatilia na kuhakikisha wanakusanya Mapato yanayotokana na Ushuru wa Huduma kutoka kwa Makampuni yanayofanya shughuli za Uchimbaji na Uchenjuaji wa Madini ya Dhahabu na Almasi katika Migodi iliyopo maeneo ya Ishokela na Mwanagwa Wilayani humu.
Akizungumza na Menejimenti ya Halmashauri mapema leo Mhe, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi amewaagiza Wakuu wa Idara na Vitengo kuhakikisha kwamba Mapato hayo yanayotokana na Ushuru wa Huduma yanakusanywa kutoka kwa Makampuni yote yanayojishughulisha na Uchimbaji na uchenjuaji wa Madini ya dhahabu na Almasi katika maeneo mbalimbali kwa kipindi chote ambacho hawajalipa ili kuweza kuboresha na kuongeza Makusanyo ya Mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mhe,Juma Sweda amesema kuwa Wamiliki wa Makampuni ya Uchimbaji na Uchenjuaji yote yanayofanya kazi katika maeneo ya Ishokela, Mwamazengo, Shilalo, Mwanangwa na Mabuki yanapaswa kulipa Mapato ya Ushuru wa Huduma kwa Halmashauri wanapofanyia kazi na kwa mujibu wa takwimu zilizopo Makampuni hayo hayalipi kabisa na matokeo yake Halmashauri imepoteza Mapato hayo kwa muda mrefu sasa, na kuwataka Watendaji wafuatilie na kuhakikisha wote wanalipa Ushuru wa mwaka 2018/2019 pamoja na madeni yote ya nyuma.
Ameeleza kuwa ameweka Mikakati ya kuyafungia kufanya kazi ya Uchimbaji Makampuni ambayo yatashindwa kukamilisha malipo ya Ushuru husika na kuwaomba Wamiliki hao kulipa mapema vinginevyo hatua za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao pamoja na kufungiwa kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo yote ya Wilaya ya Misungwi.
Mhe,Juma Sweda amewataka pia Watendaji wa Halmashauri ya Misungwi kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu wa hali ya juu pamoja kutekeleza majukumu yao kwa Weledi kwa lengo la kuleta ufanisi na kuongeza tija kazini hususan katika suala la kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya vyanzo vya ndani kwa njia ya Kielektroniki pamoja na kusimamia utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali na Wadau wengine kupitia Sekta ya Afya, Elimu, Maji, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, TASAF III, miundombinu na Maendeleo ya Jamii kwenye miradi ya Vikundi vya Wanawake ,Vijana na Wenye Ulemavu.
Ameagiza Wakuu wa Idara na Vitengo kwenda Vijijini kutembelea na kusimamia miradi ya maendeleo ya Sekta mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na mingine ipo katika hatua za ukamilishaji na kuweza kushauri na kushirikiana na Wananchi katika shughuli za ujenzi wa miradi husika na kuhakikisha inakamilika kwa wakati kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaalamu kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni na miradi itekelezwe na kukamilika kulingana na thamani ya fedha husika.
Mhe, Sweda amewataka Watendaji wote kutekeleza kikamilifu maelekezo na maagizo yanayotolewa na Viongozi wa Serikali na kuwakumbusha kuhusu maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt, John Pombe Joseph Magufuli na Makamu wa Rais Mhe, Samia Suluhu Hassan ya Wanancchi wote kufanya Usafi wa mazingira katika maeneo ya biashara na maofisini pamoja na kufanya Mazoezi ya Viungo kwa ajili ya kulinda afya na kujikinga na Magonjwa mbalimbali yasiyo ya kuambukiza , ambapo kila Mtumishi na Mwananchi anatakiwa kutekeleza maelekezo hayo kila Jumamosi ya pili pamoja na kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi,” nahitaji maelekezo hayo yaendelee kutekelezwa kwa kila Mkuu wa Idara na Vitengo kuwakumbusha Watumishi wake na Afisa Utumishi ahakikishe utekelezaji unafanyika katika Kata zote 27 kuanzia mwisho wa mwezi huu Septemba 2018 Watumishi wote wabadilike na kutimiza wajibu wao”. Alisisitiza Mkuu wa Wilaya, Juma Sweda.
Awali, katika mazungumzo yake amezitaka Idara na Vitengo vya Halmashauri kuwa na mpango madhubuti wa kutoa taarifa kwa Wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya Habari kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa na iliyokamilika ili Wananchi waweze kuona namna Serikali ya awamu ya tano inavyotekeleza na kuwapatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.